Isaiah 46

Miungu Ya Babeli

1 aBeli anasujudu hadi nchi, Nebo anainama;
sanamu zao zabebwa na wanyama wa mizigo.
Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea,
mzigo kwa waliochoka.
2 bVinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini;
hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu,
wote wanakwenda utumwani pamoja.
3 c“Nisikilizeni mimi, ee nyumba ya Yakobo,
ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli,
ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba,
nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu.
4 dHata mpaka wakati wa uzee wenu na mvi, Mimi ndiye,
Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi.
Nimewahuluku, nami nitawabeba,
nitawasaidia ninyi na kuwaokoa.

5 e“Mtanilinganisha na nani, au mtanihesabu kuwa sawa na nani?
Ni nani mtakayenifananisha naye ili tuweze kulinganishwa?
6 fWengine humwaga dhahabu kutoka kwenye mifuko yao,
na kupima fedha kwenye mizani;
huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu,
kisha huisujudia na kuiabudu.
7 gHuiinua mabegani na kuichukua;
huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo.
Wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale.
Ingawa mtu huililia, haimjibu;
haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake.

8 h“Kumbukeni hili, litieni akilini,
liwekeni moyoni, enyi waasi.
9 iKumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale;
mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine;
mimi ndimi Mungu,
wala hakuna mwingine aliye kama mimi.
10 jNi mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo,
naam, tangu zamani za kale,
mambo ambayo hayajatendeka.
Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,
nami nitatenda mapenzi yangu yote.
11 kKutoka mashariki ninaita ndege awindaye;
kutoka nchi ya mbali,
mtu atakayetimiza kusudi langu.
Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;
lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.
12 lNisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu,
ninyi mlio mbali na haki.
13 mNinaleta haki yangu karibu,
haiko mbali;
wala wokovu wangu hautachelewa.
Nitawapa Sayuni wokovu,
Israeli utukufu wangu.
Copyright information for SwhNEN